Tembo Warriors yatinga robo fainali

0
200

Timu ya Taifa ya watu wenye ulemavu (Tembo Warriors), leo imeendelea kuishangaza dunia baada ya kuifunga timu ya Japan magoli 3-1 katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa wenye ulemavu yanayoendelea nchini Uturuki.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi ndio waliiongoza kutoa hamasa na mikakati ya ushindi huo wakiungana na watanzania wanaoishi nchini Uturuki.

Akizungumza baada ya kupata ushindi huo Waziri Mchengerwa amesema, timu hiyo imeonyesha uzalendo kwa Taifa lao na kilichobaki ni kumalizia kutwaa kombe Kwa kuwa ina uwezo mkubwa wa kurejesha kombe hilo nyumbani.

Amesema serikali ipo pamoja na timu hiyo katika kila hatua, na ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuigharamia kwa kila kitu ili iendelee kufanya vizuri.

Waziri Mchengerwa ameongeza kuwa ahadi ya zawadi nono kwa timu hiyo ikiwemo shilingi milioni 40 endapo itafuzu robo fainali, shilingi milioni 80 ikifuzu kucheza nusu fainali na shilingi milioni 100 ikifanikiwa kufuzu fainali za michuano hiyo ipo palepale.

Amewataka wachezaji wa timu hiyo kuendelea kuzingatia nidhamu, umoja na kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kusema kuwa Serikali ipo kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.