Teknolojia ya VAR kutumika kombe la dunia badala ya vibendera

0
1921

Waamuzi wasaidizi katika fainali za 21 za kombe la FIFA la dunia wametakiwa kutonyanyua vibendera vyao endapo kutatokea utata wa kutambua kama kuna tukio la kuotea yaani offside na badala yake wasubiri msaada wa teknolojia ya Video -VAR ufanye kazi.

Shirikisho la soka duniani -FIFA linaamini kwamba teknolojia hiyo ya video ina msaada mkubwa katika kuwasaidia waamuzi kuamua matukio yenye utata na hii itakuwa mara ya kwanza kwa teknolojia hiyo kutumika katika fainali za kombe la FIFA la dunia.

Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi Pierluigi Collina amesema endapo mwamuzi Msaidizi hatanyanyua kibendera ifahamike kuwa atakuwa hajafanya makosa na badala yake atakuwa anaheshimu maamuzi hayo na kusubiri teknolojia ya VAR ifanye kazi yake.

Mwamuzi huyo nguli kutoka nchini Italia amesema waamuzi hao wasaidizi wametakiwa kufanya hivyo kwasababu inawezekana kutokea shambulizi la nguvu katika lango la timu mojawapo au nafasi ya kupatikana bao na endapo mwamuzi msaidizi atanyanyua kibendera basi kila kitu kitakuwa kimemalizika.

Colina amefafanua zaidi na kusema endapo mwamuzi msaidizi hatonyanyua kibendera na mchezo ukaendelea hadi bao likafungwa watatumia teknolojia ya video kupitia tukio hilo ili kujiridhisha.

Katika  michuano ya mwaka huu kutakuwa na televisheni kubwa kwenye viwanja vyote ambayo itatoa fursa kwa mashabiki kutazama namna matukio mbalimbali yanavyoamualiwa na teknolojia hiyo ikiwemo yale ya penati na kadi nyekundu.