TFF kuamua tarehe mpya Simba vs Yanga

0
318

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ameliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi kushughulika kwa haraka iwezekakavyo tarehe ya kuchezwa kwa mchezo wa watani wa jadi (Simba SC vs Yanga SC) ili kuwapa wapenzi wa soka kile walichokitarajia.

Bashungwa ametoa agizo hilo katika kikao cha pamoja kilichofanyika kati ya wizara hiyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi, Baraza la Michezo Tanzania na klabu za Simba na Yanga.

Mchezo huo namba 208 wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliokuwa uchezwe Mei 8 mwaka huu uliahirishwa kutokana na mkanganyiko uliozuka baada ya mchezo huo kusogezwa mbele kutoka saa 11:00 jioni hadi saa 1:00 jioni.

Aidha, waziri ameahidi kuitisha kikao cha pamoja ili kuondoa jakamoyo lililopo kutokana na kuwepo kutokuaminiana kati ya TFF na baadhi ya vilabu nchini, hasa klabu ya Yanga.

Ametumia nafasi hiyo kuwaomba radhi mashabiki na wapenzi wa soka nchini kufuatia kusogezwa mbele kwa saa kadhaa na baadaye kuahirishwa kwa mchezo huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu.