Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanaume, Taifa Stars, imeondoka nchini leo kuelekea Tunis, Tunisia kwa Kambi ya kujiandaa na mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu AFCON dhidi ya Algeria.
Mchezo huo utakaochezwa Septemba 7, 2023 nchini Algeria ikikumbukwa kuwa mchezo wa kwanza Tanzania ilipoteza 2-0.
Tanzania ipo kundi F pamoja na Uganda na Niger ambapo (Tanzania) inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 7 baada ya michezo mitano.
Tanzania inahitaji walau alama moja kwenye mchezo huo ili kujihakikishia nafasi kwenye mashindano hayo Afrika ambapo itafikisha alama nane ambazo haziwezi kufikiwa na Uganda yenye alama nne.
Endapo Tanzania itafungwa kwenye mchezo huo, matumaini yake ya kufuzu yatabaki kwa kuiombea Niger iifunge Uganda, au hata Uganda ikishinda, isishinde kwa tofauti ya magoli zaidi ya mawili.