Spurs wakiona cha moto kutoka kwa Leipizig

0
451

Tottenham Hotspur wakiwa nyumbani wamekiona cha mtema kuni  baada ya kunyukwa bao moja kwa bila na wabishi wa Ujerumani, RB Leipizig katika mchezo wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa suluhu kabla ya Tomo Warner kuipa ushindi muhimu wa ugenini Leipizig kwa kuifungia bao la  mkwaju wa penati katika dakika ya 58.

Katika mchezo huo Spurs inayonolewa na kocha msema hovyo Jose Mourinho ilimpoteza nyota wake Hueng Min Son aliyevunjika mkono.

Swali kubwa lililopo sasa ni je Spurs wataweza kupindua matokeo nchini Ujerumani katika mchezo ambao watawakosa kwa pamoja Son na Harry Kane.

Na huko San Siro mjini Milan – Italia, Valencia wamekutana na kipigo cha mbwa mwizi kwa kutandikwa mabao manne kwa moja na wenyeji Atlanta.

Hans Hateboer amepachika mabao mawili huku Josip Ilicic  na Remo Freuler wakifunga bao moja kila mmoja na kuipoteza Valencia ambao sasa wanahitaji miujiza ya kipekee kupindua matokeo katika mchezo wa marudiano nchini Hispania.

Atlanta wamelazimika kutumia dimba la San Siro mjini Milan kutokana na uwanja wao wa Gewiss uliopo mjini Bergamo yapata kilimotea 55 kutoka Milan kushindwa kukidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) katika matumizi ya michezo ya Ligi ya Mabingwa.