Simba yatinga robo fainali ASFC

0
268

Mabingwa Watetezi wa Kombe shirikisho (ASFC), Simba SC ya Dar es Salaam imetinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kuibanjua Kagera Suger ya Mkoani Kagera kwa mabao 2-1.

Kwa ushindi huo Simba imewafuata watani wao Yanga SC katika hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Katika mchezo huo wageni walienda mapumziko wakiwa wanaongoza bao moja lililofungwa na Erick Mwijage dakika ya 45 kwa kichwa baada ya kumalizia krosi ya beki Dickson Mhilu.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko wakimtoa Taddeo Lwanga na nafasi yake ikichukuliwa na Bernard Morrison, kuingia kwa mchezaji huyo kulibadilisha mchezo na Simba kuanza kulisakama lango la Kagera Sugar kwa mashambuli ya kustukiza.

Morrison aliwanyanyua mashabiki wa Simba dakika ya 55 akifunga bao la kusawazisha na dakika ya 67 Mshambuliaji raia wa Rwanda Meddie Kagere alipigilia msumari wa pili.

Kwa ushindi huo Simba inaungana na vigogo wa Soka nchini Yanga ambao walitinga jana hatua ya robo fainali baada ya kuwachapa Tanzania Prisons ya Mbeya bao 1-0 katika mchezo uliopigwa katika dimba la Nelson Mandela Mjini Sumbawanga.