Simba yatinga hatua ya makundi michuano ya Afrika

0
1136

Mabingwa wa soka la Tanzania Bara, klabu ya Simba imetinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika baada ya miaka 15 kupita baada ya kuinyuka timu ya Nkana FC ya Zambia mabao matatu kwa moja.

Timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi, Kariakoo imetinga hatua ya makundi baada ya kupindua matokeo ya kichapo cha mabao mawili kwa moja kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa wiki moja iliyopita nchini Zambia.

Bao la dakika ya 89 la kiungo Clatous Chama limeivusha timu hiyo baada ya mchezo huo kusomeka mabao mawili kwa moja hadi dakika ya 88 na hivyo bao hilo likaufanya mchezo huo usifike kwenye changamoto ya mikwaju ya penati.

Mara ya mwisho klabu ya Simba kutinga hatua ya makundi ilikuwa mwaka 2003 ambao ulikuwa ni miongoni mwa msimu wa mafanikio kwenye anga za kimataifa kwa klabu hiyo.

Simba inaungana na baadhi ya vilabu vingine kama Wydad Casablanca ya Morocco, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Orlando Pirates ya Afrika Kusini zilizotinga hatua hiyo pia.

Timu nyingine zilizotinga hatua hiyo ni Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini, Ismailia na Al Ahly za Misri, Lobi Stars ya Nigeria pamoja na bingwa mtetezi Esperance ya Tunisia

Droo ya hatua ya makundi itapangwa ijumaa, desemba 28 mwaka huu ambapo timu 16 zitakazotinga hatua ya makundi zitapangwa kwenye makundi manne yenye timu nne nne.