Wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya vilabu Barani Afrika, Simba SC watamenyana na Tout Puisant Mazembe Englabe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) katika Robo Fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika mapema mwezi ujao.
Katika droo iliyofanyika usiku wa jana kwenye ukumbi wa Aida Ballroom, Marriot Zamalek mjini Cairo nchini Misri, Simba SC iliwakilishwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo Swedi Nkwabi na Mtendaji Mkuu Crescentius Magori na itaanzia nyumbani katika mchezo utakaochezwa kati ya Aprili Tano na Sita kabla ya kusafiri kwenda Lubumbashi kwa mchezo wa marudiano utakaochezwa kati ya Aprili 12 na 13 mwaka huu.
Michezo mingine ya robo fainali itakuwa baina ya vinara wa Kundi D walilokuwapo Simba,- AL Ahly ya Misri ambao watamenyana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, huku CS Constantine ya Algeria ikikabiliwa na kibarua kigumu mbele ya bingwa mtetezi Esperance ya Tunisia na Horoya ya Guinea watavaana na Wydad Casablanca ya Morocco.
Endapo Simba itafanikiwa kuing’oa TP Mazembe na kutinga hatua ya nusu fainali itamenyana na mshindi kati ya CS Constantine ya Algeria na bingwa mtetezi Esperance Sportive Du Tunis ya Tunisia wakati mshindi wa robo fainali ya mchezo kati ya AL-Ahly na Mamelodi Sundowns yeye atamenyana na mshindi kati ya Horoya na Wydad Casablanca kwenye hatua ya nusu fainali
Mechi za hatua ya nusu fainali ya kwanza zitachezwa kati ya Aprili 26 na 27 na marudiano itakuwa kati ya Mei Tatu na Nne mwaka huu huku Fainali ya kwanza ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika kwa msimu wa 2018/2019 yenyewe itafanyika Mei 24 na marudiano itakuwa Mei 31.
Simba SC imetinga hatua ya robo fainali baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D kwa pointi zake tisa, nyuma ya AL Ahly iliyomaliza na pointi 10 na mbele ya JS Saoura ya Algeria iliyomaliza na pointi nane na AS Vita ya DRC iliyomaliaa na pointi saba.
Awali ya hapo Simba SC iliitoa Mbabane Swallows kwa jumla ya mabao 8 kwa moja, ikishinda manne kwa moja Dar es Salaam na nne bila Swaziland, kabla ya kwenda kuitoa na Nkana FC kwa jumla ya mabao mamne kwa matatu, ikifungwa mbili kwa moja Kitwe na kushinda tatu kwa moja Tanzania.