Timu ya Uganda ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 imeungana na wenyeji Tanzania katika kufuzu kwa michuano ya vijana itakayotimua vumbi mwezi Mei mwaka 2019.
Timu hiyo ya Uganda maarufu kama Simba Watoto wamekata tiketi hiyo baada ya kuifunga Ethiopia katika mchezo wa fainali wa mashindano ya kufuzu kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) magoli matatu kwa moja katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Iliwachukua dakika 15 Simba Watoto hao kuandika bao la kuongoza kupitia kwa Samson Kasozi, huku Abdul Wahad Iddi akiwa mwiba mkali kwa timu ya Ethopia baada ya kuiandikia Uganda magoli mawili katika kipindi cha pili, ambapo Waethiopia nao walipata goli la kufutia machozi katika dakika za lala salama kupitia kwa Wondimagegn Bunaro.
Katika mchezo wao wa nusu fainali, Uganda waliifunga timu ya Tanzania ya vijana wa umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys kwa kuwachabanga magoli matatu kwa moja, Ethiopia wao waliwafunga Rwanda katika hatua hiyo.
Serengeti Boys ambao walishafuzu kutokana na Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, wamemaliza michuano ya kufuzu katika nafasi ya tatu baada ya kuifunga Rwanda kwa mikwaju ya penati minne kwa mitatu baada ya dakika 90 kumalizika kwa vijana hao kutoshana nguvu kwa goli mbili kwa mbili.
Katika michuano hiyo Tanzania ilipata tuzo ya timu yenye nidhamu na Kelvin John amechaguliwa kuwa mchezaji bora