Siku ya kisasi, Kombe la Dunia

0
666

Ghana wanaamini Uruguay wanapaswa kuondolewa mapema kwenye kombe la Dunia kama vyombo vya mnadani nyakati za mvua.

Wanapaswa kuwafunga na kuwaondoa mashindanoni kama njia pekee ya kulipa kisasi na kufuzu 16 bora.

Suarez alidaka mpira ukiwa unaelekea nyavuni katika dakika ya 120 pale Soccer City, Afrika Kusini 2010 wakati ambao mpira ule kama ungeingia, Ghana angefuzu nusu fainali ya Kombe la Dunia, na kuwa nchi ya kwanza kutoka Afrika kufika hatua hiyo.

Hakuna picha itakayokuwa na msisimko kwao kuliko ya kuona Luis Suarez analia kwa uchungu baada ya mechi hii, na huenda atastaafu. Mwaka 2010 Suarez alilia kwa furaha ya kuipeleka nusu fainali Uruguay kwa mbinu yake ‘haramu’.

Andrew Ayew aliyelia baada ya tukio lile akiwa benchi analo jukumu la kuwaongoza wenzie dhidi ya ‘muovu’ wao Luis Suarez. Ayew peke yake kwa Ghana kati ya wale waliokuwepo mwenye uhakika wa kucheza na Suarez yupo na wenzie wengi.

Wawakilishi wengine wa Afrika Cameroon watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Brazil katika mchezo wa kufunga kundi ambao ni lazima washinde ili kufuzu kwenye hatua inayofuata huku akiombea matokeo yoyote mabovu ya Serbia na Uswisi.

Wana asilimia chache sana kufuzu kwenye hatua zinazofuata lakini mpira una maajabu yake.

Fuatilia michezo hii Desemba 2, mbashara kwa mwonekano ang’avu kabisa, yaani FULL HD, majira ya Saa 12 jioni na saa 4:00 usiku kwa lugha adhimu ya Kiswahili bila kelele kupitia TBC1, TBC Taifa na mtandao wa YouTube wa TBCOnline.