Serikali kuendelea kumsaidia Samatta

0
271

Serikali imesema kuwa itaendelea kumsaidia nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania – Taifa Stars anayechezea Klabu ya Genk ya nchini Ubelgiji Mbwana Samatta,  ili kuhakikisha kuwa anafungua milango ya uwekezaji na kuiweka juu ramani ya soka la Tanzania katika anga za Kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt  Hassan Abbasi wakati wa mazungumzo yake na Samatta na kuongeza kuwa mchezaji huyo ameonyesha njia iliyoshindwa kufikiwa na wachezaji wengi wa miaka ya nyuma waliojaribu kucheza Soka la kulipwa katika vilabu mbalimbali vya nchi za nje hususani Bara la Ulaya.

Dkt Abbasi amesema kuwa serikali ilimteua Samatta kuwa Balozi wake wa Utalii kutokana na sifa za mchezaji huyo nje ya mipaka ya Tanzania,  kwa kuwa serikali ina imani naye katika kufungua milango ya fursa za uwekezaji hususani katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.

 “Mbwana Samatta ameonyesha njia ambayo ilikuwa ndoto iliyoshindwa kutimizwa na wachezaji wengi wa zamani, hatua hii aliyofikia ni kubwa na imetokana na sifa kubwa ya nidhamu na kipaji cha mchezo huu,  hili ni funzo kwa wachezaji wetu chipukizi” amesema Dkt Abbasi.

Kwa upande wake Samatta amesema kuwa akiwa nchini Ubelgiji tayari amefanya juhudi kubwa katika kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini, ambapo mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu madaktari Watano  wa Klabu ya Genk anayoichezea nchini Ubelgiji,   wanatarajia kuja nchini kwa ajili ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii.

Amesema kuwa raia wengi wa kigeni wanatamani kuitembelea Tanzania  kutokana na kusikia na kuona uzuri wa vivutio mbalimbali vya utalii wakiwemo Wanyama, hivyo akiwa Balozi wa Utalii afanya kila liwezekanalo  kukaa karibu na viongozi na wachezaji wa klabu yake ya Genk kuwaeleza uzuri wa Tanzania ili na wao waoneshe nia ya kuitembelea Tanzania.