Serengeti Girls kuikabili Canada leo

0
180

Timu ya wasichana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls), leo inashuka dimbani katika mechi ya mwisho ya kundi D dhidi ya Canada, katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa umri huo.

Mchezo huo utapigwa katika dimba la DY Patil Navi – Mumbai nchini India majira ya saa 2 usiku saa za India sawa na saa 12: 30 jioni saa za Tanzania.

Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo alipowatembelea wakiwa kwenye mazoezi huko nchini India, Naibu waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul amewataka wachezaji hao kuingia uwanjani wakiwa na ari, kujiamini lakini pia kujua kuwa Watanzania wanahitaji kuona wanasonga mbele katika mashindano hayo ya Kombe la Dunia.

“Tanzania tunahitaji ushindi ili tusonge mbele, mchezo mliocheza juzi na Ufaransa kaongezeni kasi maana Canada pia ni wazuri, Rais Mhe. Mama Samia na Waziri Mhe. Mchengerwa wanaimani kubwa na nyie hivyo msiwaangushe.”
amesisitiza Naibu Waziri Gekul

Kwa upande wake, kocha wa Serengeti Girls,
Bakari Shime amesema wachezaji wote wako vizuri kiakili na kimwili na wapo tayari kwa mchezo wa leo ambao utakua wa kujilinda na kushambulia.

Mechi hiyo ya mwisho kwa kundi D ni lazima Tanzania ishinde au ipate sare ya aina yoyote ili isonge mbele katika hatua ya robo fainali ya kombe hilo la Dunia kwa wasichana wa umri wa chini ya miaka 17.