Samatta achukizwa na vitendo vya mashabiki wa Tanzania

0
599

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta amewataka Watanzania kuacha kuandika maneno ya kashfa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za klabu yake mpya, Aston Villa, pamoja na kurasa binafsi za wachezaji wenzake.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema kuwa anafahamu kwamba Watanzania wanatamani afanye vizuri katika klabu hiyo, lakini vitendo vya kuikashfu timu pamoja na wachezaji wenzake havimfurahishi.

“Mashabiki wa soka Tanzania nafahamu kuwa mnanipenda kijana wenu na mnapenda nifanye vizuri katika timu yangu mpya, lakini nawaomba muache kutoa maneno ya kashfa au yenye mlengo mbaya katika accounts (kurasa) za timu au wachezaji, binafsi sifurahishwi.”

Samatta alicheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya England mwishoni mwa wiki ambapo alifanikiwa kuifungia timu yake goli la kufutia machozi baada ya kupoteza kwa magoli 2-1 dhidi ya AFC Bournemouth.

Kufuatia goli hilo, Samatta ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza, na Mtanzania wa kwanza kufunga goli katika ligi hiyo pendwa zaidi duniani.