Salah aingia kwenye mgogoro na EFA

0
2484

Nyota wa timu ya Misri na klabu ya Liverpool, -Mohamed Salah ameingia kwenye mgogoro na chama soka nchini Misri (EFA) baada ya chama hicho kupuuza malalamiko yake yanayohusu kukiukwa kwa haki za matangazo.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amekishutumu chama hicho kwa kumuingiza kwenye sintofahamu na wadhamini wake ambao ni kampuni ya mawasiliano ya Vodafone baada ya EFA kutumia picha ya Salah kuitangaza kampuni ya WE ambayo ni kampuni pinzani ya Vodafone.

Akitumia mtandao wake wa kijamii wa Twitter, – Salah amesema kuwa alituma barua kadhaa kwa EFA lakini chama hicho kimezipuuza na kusema haelewi kwanini hajibiwi.

Hatua hiyo imezua tafrani nchini Misri ambapo taarifa za ndani zimeeleza kuwa mchezaji huyo anapanga kuisusia timu ya taifa ambayo mwezi Septemba mwaka huu itacheza na Niger kwenye mchezo wa kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika.

Hata hivyo EFA imekanusha suala la Salah kugomea mchezo huo kwa kusema kuwa habari hizo sio sahihi kwani Salah hajawasilisha ombi hilo.