Mshambuliaji wa kimataifa wa England, – Wayne Rooney atarejea dimbani kuitumikia timu ya taifa hilo katika mchezo maalum wa kumuaga dhidi ya Marekani baadae mwezi huu.
Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 33, anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika taifa hilo akiwa amefunga mabao 53.
Mara ya mwisho kuitumikia timu ya taifa ya England ilikuwa mwezi Novemba mwaka 2016, ambapo timu hiyo ilipata ushindi wa mabao matatu kwa bila dhidi Scotland.
Mchezo huo utakaochezwa Novemba 15 mwaka huu kwenye dimba la Wembley jijini London utakuwa wa 120 kwa Rooney kuitumikia timu ya taifa na tayari mechi hiyo imepewa jina la taasisi ya kimataifa ya Wayne Rooney yaani The Wayne Rooney Foundation international.
Chama Cha Soka cha England (FA) kimesema kuwa hiyo ni nafasi pekee ya kumuaga kwa heshima nguli huyo na kwamba uwanja wa Wembley utapambwa kwa rangi za dhahabu zilizopo kwenye taasisi hiyo ya kimataifa ya Rooney.
Kwa upande wake Rooney amesema kuwa anajisikia fahari kuichezea tena timu ya taifa na kumshukuru kocha wa kikosi hicho Gareth Southgate pamoja FA kwa kumuita kwenye mchezo huo.