Ronaldo kuvaa tena namba 7 Man U

0
2221

Mchezaji Edinson Cavani ameachia uzi wake wa namba saba na kumpatia Christiano Ronaldo, aliyesainiwa kwa mara nyingine tena na klabu ya Manchester United ya nchini Uingereza.

Ronaldo anayetamba kwa kuwa moja kati ya wachezaji bora wa soka duniani, amejizolea umaarufu zaidi kwa jezi yake ya namba saba na hashtag ya #CR7.

Aliachana na klabu ya Juventus ya nchini Italia na kusainiwa na Man U mwezi Agosti mwaka huu, huku tayari jezi namba saba kwa Man U ikiwa inavaliwa na Cavani ambaye alijitolea kumpa namba hiyo Ronaldo.

“Sikudhani kama ingewezekana kupata tena shati namba saba. Kwa hivo ningependa kusema asante kubwa kwa Edi (Cavani) kwa ishara hii nzuri,” amesema Ronaldo.

Kwa sasa Cavani atakuwa anavaa namba 21 baada ya Dan James aliyekuwa akivaa namba hiyo kuhamia Leeds United.

Namba hiyo inakuwa ni ‘bonus’ kwa Cavani ambaye anavaa namba 21 katika timu yake ya Taifa ya Uruguay.

Jezi namba saba imekuwa ikivaliwa na wachezaji mashuhuri wa klabu ya Man U ikiwemo David Beckham, Eric Cantona, Bryan Robson na George Best.

Ronaldo kwa sasa ndiye mtu mwenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao wa Instagram, akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 330.