Rais Magufuli ataka ushindi kwa Stars

0
2410

 

Rais John Magufuli ametoa wito kwa wachezaji wa timu ya Taifa  ya mpira wa miguu – Taifa Stars kujituma ili timu hiyo iweze kufanya vizuri katika michezo iliyosalia ya kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2019 nchini Cameroon.

Rais Magufuli ametoa wito huo Ikulu jijini Dar es salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji wa Taifa Stars, viongozi wa timu hiyo wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), – Walece Karia na viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), mazungumzo yaliyohudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Augustine Mahiga.

Amesema kuwa Watanzania wengi wamekata tamaa kushabikia timu za ndani kutokana na timu hizo kufanya vibaya katika mashindano mbalimbali, hivyo ni vema wachezaji wa Stars wakaamsha ari ya Watanzania ya kushabikia timu yao ambayo haijawahi kushiriki katika fainali hizo kwa muda wa  miaka 38.

Rais Magufuli ametumia mkutano huo kuwataka viongozi wa vyama vya michezo nchini kutumia pesa kwa manufaa ya timu zao na si kujinufaisha, kwa kuwa kwa muda mrefu viongozi hao wamekua wakijinufaisha wenyewe na hivyo kuwakatisha tamaa wachezaji.

Amewataka viongozi hao kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa na na kuongeza kuwa katika uongozi wake atahakikisha vitendo vya rushwa vinakomeshwa katika sekta ya michezo.

Rais Magufuli ameukabidhi uongozi wa Taisa Stars shilingi milioni hamsini ikiwa ni mchango wake kwa timu hiyo inayoajiandaa kuweka kambi nje ya nchi kwa ajili ya kuajiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho na Uganda kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali hizo za kombe la Mataifa ya Afrika.