Plate walalamikia mtanange kufanyika Santiago Bernabeu

0
1591

Mtendaji Mkuu wa klabu ya River Plate, –  Marcelo Gallardo amesema  kuwa kitendo cha mchezo wa fainali ya pili ya michuano ya ligi ya mabingwa Barani Amerika ya Kusini baina yao na mahasimu wao wakubwa Bocca Juniors maarufu kama Copa Libertadores kuhamishiwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu jijini Madrid nchini Hispania ni ukatili kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Mchezo wa fainali ya kwanza uliowakutanisha wababe hao wa soka la Argentina,  ulimalizika kwa sare ya mabao  mawili kwa mawili na mchezo wa marudiano uliahirishwa mara mbili baada ya mashabiki wa River Plate kuwashambulia wachezaji wa Bocca Juniors na kuwasababishia majeraha.

Akizungumza baada ya River Plate kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Gimnasia La Plata  kwenye mchezo wa ligi uliofanyika Jumatatu Disemba tatu, Gallardo amesema kuwa mchezo huo kuchezwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu sio uungwana kwani kunawanyima faida ya kucheza nyumbani na kamwe hawatasahau tukio hilo.

Katika mchezo huo wa marudiano utakaochezwa Jumapili Disemba Tisa, kila timu itapewa tiketi  Elfu 25 lakini tiketi Elfu Tano tu kati ya hizo ndio zitauzwa kwa mashabiki nchini Argentina ukiwa ni mpango wa kudhibiti vurugu zinazoweza kuandaliwa na mashabiki kutoka nchini humo.

Serikali ya Argentina imesema kuwa inashirikiana kwa karibu na serikali ya Hispania ili kuhakikisha hakuna uwezekano wa kutokea vurugu zozote kwenye mchezo huo.