Patrice Motsepe Rais mpya CAF

0
265

Mmiliki wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, –  Patrice Motsepe, amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF)  akirithi mikoba ya mtangulizi wake Ahmad Ahmad ambaye alifungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kujihusisha na soka kwa muda wa miaka miwili.

Motsepe  ataongoza Shirikisho hilo akisaidiwa na Makamu wa Rais wawili ambao ni Augustin Senghor wa Senegal na Ahmed Yahya raia wa Mauritania.

Jacques Anouma ambaye ni raia wa Ivory Coast ametajwa kama mshauri maalum wa CAF.

Motsepe amepitishwa kushika wadhifa huo katika uchaguzi  ambao haukuwa na mpinzani, baada ya mgombea Jacques Anouma kujitoa siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Motsepe anakuwa raia wa kwanza kutoka Afrika Kusini kuongoza Shirikisho la Soka Barani Afrika,  akifuata nyayo za viongozi saba waliowahi kuongoza Shirikisho hilo wakitokea mataifa ya Misri, Sudan, Ethiopia, Cameroon na Madagascar.

Tofauti na viongozi wengine waliomtangulia,  Motsepe hana historia ya kuongoza vyama ama shirikisho la soka,  lakini kinachomuunganisha na mchezo huo ni umiliki wake wa klabu ya Mamelodi Sundowns ambayo ni mabingwa wa Afrika kwa mwaka 2016.

Patrice Motsepe mwenye umri wa miaka 59 alianza kazi zake kama Mwanasheria, baadaye akajihusisha na kazi ya uchimbaji wa madini.

Jarida la Forbes linamtaja Patrice Motsepe kuwa na utajiri unaofikia dola bilioni 2.9 za Kimarekani.