Benki ya NMB imegawa vifaa kwa timu za Bunge ikiwa ni maandalizi ya bonanza maalum litakalozihusisha timu za Bunge na wafanyakazi wa benki hiyo.
Akikabidhi vifaa hivyo jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema, wanatarajia kuona wabunge pamoja na wafanyakazi wa benki yake wakifurahi pamoja katika michezo mbalimbali siku ya Jumamosi.
Zaipuna amesema, bonanza hilo ni muendelezo wa mabonanza mengine ambayo yamefanyika katika miaka ya nyuma ambapo lengo kuu ni kushiriki katika mazoezi kuelekea msimu huu wa mbio za NMB zinazotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Mwenyekiti wa Bunge Sports Abbas Tarimba, amewataka wachezaji wa timu zote za bunge kujiandaa kikamilifu kushiriki bonanza hilo ambalo litahusisha michezo mbalimbali.