Njoya ahaidi kuendeleza soka la Cameroon

0
1557

Rais mpya wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini Cameroon (FECAFOOT), – Seidou Njoya amesema kuwa lengo lake ni kurejesha uaminifu kwenye soka la nchi hiyo.

Njoya ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku mbili tu tangu achaguliwe kuwa Rais wa FECAFOOT na kuongeza kuwa atafanikisha lengo hilo kwa kuupa kipaumbele uwazi katika uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu nchini Cameroon.

FECAFOOT imekuwa haina Rais tangu mwaka 2013 baada ya aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo Iya Mohammed kuhukumiwa kifungo jela, hali iliyosababisha shirikisho hilo kuendeshwa na kamati maalumu kwa kipindi cha miaka mitano.

Njoya amesema kuwa baada ya miaka mitano ya mvutano kwenye soka la nchi hiyo, umefika wakati wa kufanya mabadiliko kwa kufuata weledi na utawala bora kwenye soka.

Kwenye uchaguzi uliomuingiza madarakani Njoya siku ya Jumatano, kigogo huyo mwenye umri wa miaka 57 alipata kura 46 kati ya 66 huku mpinzani wake wa karibu akiwa mlinda mlango wa zamani wa timu ya Taifa ya Cameroon, -Joseph Bell akipata kura 17.