Ndayiragije aita 30 kujiandaa na CHAN

0
197

Jumla ya wachezaji 30 wameitwa kwenye kikosi cha awali cha timu ya taifa ya soka ya Tanzania ( TAIFA STARS) kwa ajili ya michuano ya CHAN itayofanyika nchini Cameroon kuanzia katikati ya mwezi ujao wa January 2021.

Katika kikosi hicho kilichoitwa na kocha Etienne Ndayiragije amewatema baadhi ya nyota waliozoeleka kama kiungo Jonas Mkude wa Simba ambae jana alisimamishwa na timu yake ya Msimbazi kwa kosa la utovu wa Nidhamu.

Wengine walioachwa kwenye kikosi hicho ni mlinzi wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin, Salum Aboubakari na kipa wa Yanga Metacha Mnata.

Jumla ya wachezaji wapya sita wameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho wakiongozwa na Lucas Kikoti wa Namungo FC, makipa wa Abdultwalib Mushery wa Mtibwa Sugar na Dan Mgore wa Biashara United ya Mara na wachezaji sita toka timu za vijana za chini ya miaka 17 na 20.

Pia Ndayiragije amemrejesha kikosini mlinzi kongwe wa Azam FC Agrey Morris ili kuimarisha sehemu ya ulinzi wa kati kwenye kikosi chake kushirikiana na Erasto Nyoni na kijana Bakari Mwamnyeto.

Timu hiyo itaingia kambini January mosi 2021 na itacheza michezo miwili ya kirafiki na DR CONGO kabla ya kuelekea nchini Cameroon tayari kwa michuano hiyo ya CHAN.