NBA kutimua vumbi karibuni

0
2328

Nchini Marekani imechezwa michezo mitatu ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini humo – NBA itakayoaanza kuunguruma rasmi Oktoba 16 mwaka huu.

New Orlan Pelicans wakiwa nyumbani Smoothie King Center- Los Angeles wamekula kichapo kwa kunyukwa alama 134 kwa 119 na Toronto Raptors katika mchezo ambao Pascal Siakami ameibuka shujaa kwa kuifungia timu yake ya Raptors alama 21 na kucheza mipira iliyorudi yaani Rebounds 12.

Licha ya nyota wa Pelicans, – Antony Davis, Julius Randle na Nikola Mirotic kwa pamoja kufunga alama 71 bado hazikutosha kuipa timu yao ushindi mbele ya Raptors waliotawala sehemu kubwa ya mchezo huo.

Huko Golden One Center mjini Sacramento – California, wenyeji Sacramento Kings wamekiona cha moto baada ya kutandikwa alama 132 kwa 93 na Utah Jazz.

Rudy Gobert amefunga alama 18 na kucheza Rebounds saba zilizochagiza ushindi wa Jazz wakiwa ugenini na kuibua matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo kufanya vema kwenye msimu unaokuja.

Mchezo wa mwisho umechezwa kwenye dimba la Stapeles mjini Los Angeles – California,  kwa timu ya Haifa Macabi kuchezea kichapo baada ya kula mweleka wa alama 124 kwa 76 kutoka kwa wenyeji Los Angeles Clippers.

Boban Marjanovic ameifungia Clippers alama 18 na kucheza Rebounds 12 zilizochagiza ushindi huo mbele ya Maccabi iliyokuwa ikiongozwa na Roman Sorkin aliyefunga alama 12 na kucheza Rebounds tatu.