Mwili wa aliyekuwa mchezaji wa Chelsea na vilabu mbalimbali barani Ulaya Christian Atsu umewasili mjini Accra, Ghana usiku wa kuamkia leo baada ya kukutwa amefariki dunia siku 12 baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria.
Mwili wa mwanandinga huyo umepokewa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kotoko na viongozi mbalimbali wa Taifa hilo, huku Jeshi la Ghana likihusika katika kuupokea na kuuhifadhi mwili wa Atsu.
Kifo cha Atsu kilitangazwa Jumamosi na wakala wake Nana Sechere, ambaye alisema mwili wa mchezaji huyo ulipatikana siku 12 baada ya maafa hayo kukumba Uturuki na Syria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu elfu 44.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ghana, aliyekuwa na umri wa miaka 31 amewahi kuichezea klabu ya Chelsea, Everton na Porto na mpaka umauti unamfika alikuwa akiichezea timu ya Ligi Kuu ya Uturuki ya Hatayspor.