Bondia namba moja wa uzito wa kati nchini Hassan Mwakinyo anatarajia kupanda ulingoni mwezi Februari mwaka huu kucheza pambano la kimataifa lililopangwa kufanyika jijini Mwanza.
Hata hivyo bado jina la mpinzani wake halijawekwa wazi na pia haijajulikana kama litakuwa ni pambano la ubingwa ama la kirafiki.
Akizungumza na TBC katika kipindi cha Jambo Tanzania, Muandaaji wa mapambano ya ngumi za kulipwa nchini Selemani Semunyu amesema mwaka huu wamedhamiria kupeleka mapambano ya ngumi mikoani na wanaanza na pambano la Hassan Mwakinyo kulipeleka mkoani Mwanza.
“Kwa mwaka huu tumekusudia kutanua zaidi mchezo huu wa ngumi hadi mikoani na kwa sasa tunaanza na pambano la bondia namba moja nchini litakalofanyika mkoani Mwanza mwezi Februari,” amesema Semunyu.
Ametoa rai kwa Wadau wa ngumi kujitokeza kuunga mkono maandalizi ya mapambano nchini.
“Niwaombe Wadau wajitokeze kwa wingi kuunga mkono juhudi hizi, kwani dhamira yetu ni kuandaa mapambano mengi mikoani kwa mwaka huu,” amesema Semunyu.