Mshindi Ballon D’or kutangazwa leo

0
2325

Mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2018 ya Ballon D’or atatangazwa baadaye hii leo katika hafla itakayofanyika jijini Paris nchini Ufaransa.

Nahodha wa timu ya Taifa ya  Croatia anayechezea Real Madrid, – Luka Modric anapigiwa chapuo kubwa ya kutwaa tuzo hiyo na kumaliza utawala wa nyota wawili Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ambao wamekuwa wakipokezana tuzo hiyo kwa kipindi cha miaka kumi mfululizo.

Nahodha wa FC Barcelona, – Lionel Messi na mshambuliaji wa Juventus, – Cristiano Ronaldo wameshinda tuzo hiyo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kila mmoja akishinda mara tano ambapo mchezaji wa mwisho kushinda tuzo hiyo kando ya wawili hao alikuwa Ricardo Kaka aliyeshinda tuzo hiyo mwaka 2007 akiitumikia AC Milan ya Italia.

Hata hivyo,  Luka Modric anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo hiyo baada ya mwezi Septemba mwaka huu kushinda tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa FIFA, tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya na tuzo ya mchezaji bora wa fainali za kombe la FIFA la dunia zilizofanyika mwezi Juni hadi Julai mwaka huu nchini Russia.

Tangu mwaka 1956 , Jarida la France Football limekuwa likitoa tuzo hiyo yenye thamani kubwa zaidi duniani kwa mchezaji bora wa kiume kila mwaka na mwaka huu wameongeza tuzo kwa upande wa mchezaji bora wa kike na mchezaji bora kijana.