Mourinho awasifu wachezaji wake

0
1904

Kocha wa timu ya Manchester United, – Jose Mourinho amesema kuwa wachezaji wa timu hiyo walijituma kwa kiwango cha juu katika mchezo wao dhidi ya Arsenal uliomalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili.

Amesema kuwa mchezo  huo  katika Ligi Kuu ya England uliopigwa kwenye dimba la Old Trafford ulikua ukisubiriwa kwa hamu kubwa  na mashabiki kote duniani, hivyo ilikua ni lazima kucheza kufa na kupona ili kuweza kupata matokeo mazuri.

Kwa siku kadhaa kabla ya mpambana huo, mashabiki wa pande zote mbili za timu ya Manchester United na Arsenal walikua wakitambiana ambapo kila upande ulijinasibu kushinda.

Arsenal ndio walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya 26 kupitia kwa mchezaji wake  Shkodran Mustafi na dakika nne baadae Man U wakasawazisha kupitia kwa mchezaji Anthony Martial ambapo  hadi dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza zinamalizika timu hizo zilitoka sare ya bao  moja kwa moja.

Katika kipindi cha pili,  mchezaji Alexandre Lacazette wa Arsenal  alifunga goli la pili kwenye dakika 68, lakini ndani ya dakika moja mchezaji wa Jesse Lingard akasawazisha.

Kwa sare hiyo, Arsenal imefikisha alama 31 ikiwa nafasi ya tano huku Man U ikifikisha alama 23 na kuwa nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu England inayoongozwa na Manchester City.

Nayo Wolverhampton Wanderers imeiduwaza Chelsea baada ya kuitandika mabao mawili kwa moja.

Chelsea ndiyo ilikuwa ya kwanza kupachika bao kupitia kwa Ruben Loftus-Cheek katika  dakika ya 18 mchezo huo.

Wolves walipambana katika kipindi cha pili ambapo walisawazisha dakika ya 59 kupitia kwa Raul Jimenez,  lakini Diogo Jota akapeleka kilio Chelsea  katika dakika ya 63  baada ya kupachika goli la ushindi.

Liverpool nao wakiwa ugenini wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuitandika Burnely magoli matatu kwa moja.

Burnely ndio walikuwa wa kwanza kupachika goli la kuongoza kwenye dakika ya 54 kupitia kwa mchezaji Jack Cork.

Liverpool wakapambana kuondoa aibu wakasawazisha kupitia kwa Roberto Firmino  na magoli ya mawili ya ushindi yakafungwa na wachezaji James Milner  na Xherdan Shaqiri.

Liverpool wanaendelea kushikilia nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya  England wakiwa na alama 39.