Mkhitaryan kutokwenda Baku

0
280

Kiungo wa klabu ya Arsenal ya nchini England, – Henrikh Mkhitaryan hatakuwemo katika kikosi kitakachoshuka dimbani kwenye mchezo wa fainali wa michuano ya Europa  dhidi ya Chelsea Mei 29 mwaka huu mjini Baku Azerbaijan.

Taarifa kutoka jijini London zinadokeza kuwa sababu za kiusalama  zimesababisha Mikh ambaye ni kiungo mshambuliaji kutokuwemo katika kikosi hicho.

Uhusiano mbaya wa kisiasa baina ya Azerbaijan na Armenia ni sababu kubwa ya Mkhitaryan kuukosa mchezo huo.

Mkhitaryan ambaye ni raia wa Armenia amesema kuwa ulikuwa ni uamuzi mgumu na inauma kuukosa mchezo wa fainali ya kihistoria kwani  ni adimu kupata fursa ya kucheza mechi kama hizo.

Uongozi wa klabu ya Arsenal umedokeza kuwa umeandika barua kwa Shirikisho la Soka Barani Ulaya kuhusu tahadhari hiyo huku shirikisho hilo likitoa hakikisho la usalama wa wachezaji wote watakaocheza fainali mjini Baku.

Mwaka 2015 alipokuwa Borussia Dortmund ya nchini Ujerumani, Mikh hakusafiri kwenda  Azerbaijan kucheza dhidi ya Gabala FC,  pia akiwa Arsenal hakucheza dhidi ya FK Qarabag mwezi Oktoba mwaka 2018 kwa sababu za kiusalama.

Endapo itashinda fainali hiyo, Arsenal itakuwa ni mara ya kwanza kutwaa taji la Ulaya tangu ilipofanya hivyo mwaka 1994 ilipotwaa kombe la Washindi Ulaya pia itakuwa imejikatia tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya (UEFA) msimu ujao.