Mechi za nusu fainali ya CHAN kupigwa leo

0
363

Michezo ya nusu fainali za michuano ya CHAN mwaka 2021 zitachezwa leo huko nchini Cameroon ambapo washindi watafuzu kucheza fainali Jumapili Februari 7, mwaka huu.

Nusu fainali ya kwanza itakuwa baina miamba miwili ya Afrika Magharibi ambapo Mali maarufu The Eagle itapambana na Guinea (Syli Nationale).

Mchezo huo utaanza saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki sawa na saa 10:00 jioni saa za Cameroon.

Kocha wa Mali, Nouhoun Diane amesema wamejipanga vyema na atatumia udhaifu aliouona kwenye kikosi cha Guinea kushinda mchezo huo. Naye kocha wa Guinea, Kanfory Banguoura amesema wamejipanga kushinda mchezo huo ingawa watakuwa na presha kuwa kwa sababu Rais wao Alpha Conde atakuwa akiutazama mchezo huo.

Mchezo wa pili wa nusu fainali utachezwa saa nne usiku kwa saa za hapa nyumbani ambapo mabingwa watetezi Morocco watapambana na wenyeji Cameroon.

Hiyo ni vita ya Simba wawili ambapo Cameroon wao wanajiita Simba Wasiofugika huku Morocco wao wakiijita Simba toka Milima ya Atlas.

Mchezo huo wa pili baina ya Cameroon na Morocco utakuwa na upinzani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili walioonesha kwenye michezo iliyopita.