Mchezo wa Barcelona na Girona wazua utata

0
1952

Klabu ya Real Madrid imepinga mchezo wa ligi daraja la kwanza nchini Hispania maarufu kama  LA Liga kati ya mahasimu zao wakubwa FC Barcelona na Girona kuchezwa Marekani.

Awali bodi ya LA Liga iliomba ruhusa kwa chama cha soka nchini Hispania (RFEF) ili mchezo huo uchezwe mjini Miami  Januari 26  mwaka  2019 lakini katika barua yake kwa Chama Cha Soka nchini Hispania,  Madrid imesema kuwa ni sheria kwa timu kucheza katika viwanja vyao vya  nyumbani na ugenini kwa ajili ya kuitendea haki na usawa ligi ya LA Liga.

Rais wa chama cha soka nchini Hispania, – Luis Rubiales amepinga mchezo huo kuchezwa nchini Marekani kama ambavyo wamefanya umoja wa wachezaji wa Hispania (AFE) huku bodi ya Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA), Shirikisho la Soka Nchini Marekani na Shirikisho la soka Amerika Kaskazini, Kati  na Visiwa vya Carribean nao wakitakiwa kutoa ruhusa kwa mchezo huo kufanyika.

Katika barua yao Real wamesema kwanza wanataka ifahamike kuwa wao hawajawahi kutaarifiwa kuwa LA Liga  wameomba mchezo huo kuchezwa wala hawakuwa na tetesi yoyote kuhusu suala hilo na wala hawakuwahi kuulizwa kuhusu maoni yao kwenye mpango huo na kwamba mpango huo utaathiri mashindano.

Mchezo huo unaopendekezwa Girona,  wanaotoka mji wa Catalan ulipo maili sitini kutoka  kaskazini mwa Barcelona ndiyo watakuwa nyumbani na unatarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Hard Rock  mjini  Miami  Januari 26 mwaka  2019 kama sehemu ya kukidhi matakwa ya haki ya matangazo ya televisheni.