Mamluki SHIMUTA kuchukuliwa hatua

0
903

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe ametangaza kuwachukulia hatua Wanamichezo wasiokuwa Wafanyakazi “Mamluki” wanaoshiriki Mashindano ya Michezo kwa Wafanyakazi (SHIMUTA) na (SHIMIWI) endapo watabainika.


Dkt Mwakyembe ametangaza hatua hiyo jijini Mwanza, wakati akifungua rasmi michezo ya Mashirika ya Umma na Binafsi (SHIMUTA) kwa niaba ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mlezi wa mashindano hayo.


Amesisitiza kuwa, lengo la kuwepo kwa mashindano hayo ni kuimarisha afya za Wafanyakazi, kubadilishana uzoefu pamoja na kutangaza Taasisi zao, hivyo vi vema walengwa wakashiriki kikamilifu.


“Kuna hili suala la Wachezaji ambao sio Wafanyakazi maarufu kwa jina la Mamluki kushiriki karika michezo hii,tena nakumbuka kuna kiongozi aliwahi kuwaita viongeza nguvu bambikizi, hapa sio mahala pao, nawataka wajiondoe mapema maana tukiwabaini wao pamoja na Taasisi zao tutawachukila hatua”, amesema Waziri Mwakyembe.

Ameongeza kuwa, mwaka 2018 mashindano hayo ya SHIMUTA yalipofanyika jijini Dodoma, Makamu wa Rais hakuridhishwa na idadi ya washiriki kutokana na idadi ya Kampuni na Mashirika yaliyopo nchini na kuagiza ufanyike mkutano kujua sababu na kuzipatia majibu, na kwamba mkutano huo umezaa matunda kwa kuwa mwaka huu idadi imeongezeka kutoka Mashirika 26 hadi 46.

Mashindano hayo yalianza rasmi Novemba 27 mwaka huu.