Makundi kombe la Shirikisho yapangwa

0
1090

Timu tatu za mpira wa miguu kutoka nchini Morocco zimepangwa kwenye kundi moja katika hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Barani Afrika katika droo iliyofanyika Januari 21 mwaka huu.

Katika kundi A, bingwa mtetezi wa michuano hiyo Raja Casablanca wamepangwa na timu ya Renaissance Berkane na Hassania Agadir,  wakiwa pamoja na timu ya As Otoho Oyo ya Congo Brazzaville.

Kundi  B zipo timu mbili za Tunisia,  ambazo ni bingwa wa kihistoria wa michuano hiyo CS Sfaxien na bingwa mara mbili wa kombe hilo la Shirikisho Barani Afrika, -Etoile Du Sahel.

Timu nyingine mbili zinazounda kundi hilo ni Salitas ya Burkina Faso  na Enugu Rangers kutoka nchini Nigeria.

Nalo  kundi C, timu ya Nkana FC ya Zambia itacheza na Zesco United pamoja na timu za Al Hilal ya Sudan na miamba ya Asante Kotoko ya nchini Ghana.

Kundi la  D linaundwa na timu za Zamalek ya Misri, Hussein Dey ya Algeria, Petro Atletico ya Angola na Gor Mahia kutoka  nchini Kenya.

Hatua ya makundi ya michuano hiyo itaanza mwezi Februari mwaka huu  ambapo michezo mitatu itapigwa ndani ya kipindi cha mwezi huu huku michezo ya marudiano ikichezwa mwezi Machi.