Majaliwa: Michezo na Sanaa viwanufahishe wahusika na Taifa

0
187

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa moja ya lengo la Serikali ni kuhakikisha michezo na sanaa nyingine zinakuwa na tija kwa wahusika na Taifa kwa ujumla, hivyo lazima uwekezaji wa makusudi ufanyike.

Akizindua mashindano ya
Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) mkoani Mtwara, Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuandaa mpango mkakati kwa ajili ya kuendeleza michezo mashuleni pamoja na kurejesha mafunzo ya michezo na sanaa katika vyuo vya Butimba na Mtwara.

Waziri Mkuu ametumia jukwaa hilo kueleza hatua ambazo tayari zimeshachukuliwa na Serikali kuboresha michezo na sanaa nchini na mipango ijayo ambayo ni kuboresha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA, kuboresha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, kuimarisha utendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chama cha Hskimiliki Tanzania (COSOTA) na Bodi ya Filamu Tanzania.

Amewakosoa wanaochukulia kuwa michezo na sanaa ni sawa na kupoteza muda, huku akisema sekta hiyo imeiletea nchi fahari kubwa kwa uwekezaji uliofanyika na kuitambulisha nchi kimataifa kupitia kwa Watanzania kama Mbwana Samatta, Diamond Platnumz, Alikiba, Kelvin John na wengine wengi.

Waziri Mkuu Majaliwa amewataka Wanafunzi waliopata nafasi ya kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kuwa wasiishie ngazi hiyo, bali wajitume na kuhakikisha wanaendeleza vipaji vyao na kufika mbali.

Pia amewatia moyo waliokosa nafasi kutokukata tamaa, kwani mashindano hayo ni endelevu kila mwaka.

Mashindano hayo yanayoanza leo mkoani Mtwara na kufikia tamati Julai 3 mwaka huu, yanahusisha michezo 10 na kushirikisha Wanafunzi 7,400.

Kaulimbiu ya mashindano hayo kwa mwaka huu ni Michezo, Sanaa na Taaluma kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda.