Madrid mbabe kwa Ajax

0
737

Bingwa mtetezi wa michuano ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya Real Madrid wakiwa ugenini nchini Uholanzi kwenye dimba la Johan Cruijff Arena wametakata kwa ushindi wa mabao mawili kwa bila dhidi ya wenyeji wao Ajax Amsterdam.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa  Ustaadhi Karim Benzema aliipatia Real Madrid bao la kuongoza katika dakika ya 60 na kisha Ajax wakachomoa bao hilo kupitia kwa kinda wa kimataifa wa Morocco,- Hakim Ziyech katika dakika ya 75.

Zikiwa zimesalia dakika Tatu mchezo kumalizika,  Marco Asensio aliifungia Real Madrid bao la pili na la ushindi linaloifanya Madrid kunufaika na ushindi wa ugenini kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki mbili baadae kwenye dimba la Santiago Bernabeu.

Huko London nchini Uingereza , watanashati Tottenham Hotspur wakiwa katika dimba lao la nyumbani la Wembley, wamechomoza na ushindi mnono wa mabao Matatu kwa Bila dhidi ya wabishi Borussia Dortmund kutoka nchini Ujerumani.

Mkorea Heung-Min Son ndiYe aliyeanza kuwapatia Spurs bao la kuongoza katika dakika ya 47 ya mchezo kabla ya beki Jan Vertonghen kuongeza bao la pili katika dakika ya 83 na kisha mshambuliaji raia wa Hispania, Fernando Llorente akahitimisha kazi kwa kupachika bao la tatu katika dakika ya 86.

Michezo mingine ya hatua ya mtoano kwenye michuano hiyo ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya itaendelea Februari 19 mwaka huu  ambapo majogoo wa jiji Liverpool watakuwa wenyeji wa miamba ya Ujerumani, – FC Bayern Munichen huku Olympic Lyon ya Ufaransa wakiwaalika FC Barcelona.

Februari 20, vijana wa Diego Simeoni, -Atletico Madrid watakuwa nyumbani Wander Metropolitano kukialika kibibi kizee cha Turin,- Juventus, wakati Schalke 04 ya Ujerumani wakiwapokea Manchester City pale Veltins Arena.