Maandalizi yapamba moto, mpambano Simba na Yanga

0
219

Maandalizi katika uwanja wa Lake Tanganyika uliopo mkoani Kigoma, kwa ajili ya fainali za kombe la Shirikisho baina ya watani wa jadi Simba na Yanga yamekamilika.

Katibu wa chama cha soka mkoa wa Kigoma, Omary Gindi ameiambia TBC kuwa kinachofanyika sasa ni kupanga majukwaa ya mashabiki kulingana na bei za tiketi zao na kugawa majukwaa kwa ajili ya mashabiki wa timu zote mbili na lile la mzunguko.

“Timu zote na wageni wote mashuhuri tumeshawawekea mazingira mazuri ya malazi, hoteli zimeandaliwa na usalama wa wageni wote watakaokuwa hapa Kigoma ni wa uhakika.” Amesema Gindi

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma, Fredinandi Firimbi amesema wamejipanga vizuri kupokea ugeni, pamoja na kutumia ugeni huo kuwa fursa ya kuongeza kipato kwa Wakazi wa mkoa wa Kigoma.

“Tumeshirikiana na chama cha soka mkoa wa Kigoma kufanikisha maandalizi yote, na tunaamini mchezo huo wa Simba na Yanga utafungua fursa nyingi kwa Wananchi wa Kigoma.” Amesema Firimbi

Mpambano wa fainali za kombe la Shirikisho kati ya timu za Simba na Yanga zote za mkoani Dar es Salaam unatarajiwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu mkoani Kigoma, mpambano utatangazwa kupitia redio ya TBC Taifa na katika mitandao ya kijamii ya TBCOnline.