Maajabu ya Uwanja wa 974 nchini Qatar

0
760

Mchezo wa hatua ya 16 bora wa Kombe la Dunia 2022 kati ya Brazil na Korea Kusini ulikuwa mchezo wa saba na wa mwisho kupigwa katika Uwanja wa 974, ambao umekuwa kivutio kwa maelfu ya watu.

Uwanja huo wa kipekee ulio pembezoni mwa maji ukikupa mandhari nzuri ya jiji la Doha umejengwa kwa kutumia makasha ya kusafirishia mizigo kwenye meli (standard certified shipping containers) 974, ukiakisi uwepo wa bandari iliyopo karibu na historia ya viwanda ya eneo hilo.

Idadi ya makasha yaliyotumika kujenga uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 44,089 ndio chanzo cha jina la uwanja huo.

Baada ya kutumika, uwanja huo utavunjwa, na makasha hayo kutumika sehemu nyingine kujenga uwanja wenye uwezo huo, au kujenga viwanja vidogo kwa matumizi mbalimbali.

Kwa matumizi ya makasha, uwanja huo umepunguza gharama za ujenzi na kupunguza matumizi ya maji kwa asilimia 40.