Liverpool yapata kichapo

0
2010

Timu ya Liverpool imepata kichapo cha tatu mfululizo kwa mara ya kwanza katika historia yake kwenye michezo ya ugenini ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya baada ya kunyukwa mabao mawili kwa nunge na Red Star Belgrade kwenye mchezo wa kundi C.

Msimu uliopita Liverpool ilinyukwa mabao manne kwa mawili na AS Roma kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali ya ligi hiyo ambapo pamoja na kufungwa, ilitinga fainali kwa faida ya ushindi wa mabao matano kwa nunge ilioupata kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Msimu huu wameuanza kwa kichapo kwenye mchezo wa ugenini walipokubali kipigo cha bao moja kwa sifuri jijini Naples walipocheza na Napoli huku mchezo wa tatu ukiwa ni wa usiku wa kuamkia leo Novemba saba waliopoteza mbele ya Red Star Belgrade ya Serbia.

Mabao mawili ya mshambuliaji Milan Pavkov wa Red Star katika dakika za 22 na 29 yamewazamisha majogoo hao wa jiji na kulifanya kundi lao la C kuwa wazi kwa kila timu kusonga hatua ya mtoano baada ya Napoli na PSG kutoshana nguvu.

Napoli wao wakiwa nyumbani kwenye dimba la San Paolo walilazimika kutoka nyuma ili kusawazisha bao la Juan Bernet wa Paris Saint Germain aliyefunga katika dakika ya 45 huku Lorenzo Insigne akiisawazishia Napoli kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 63.

Katika matokeo ya michezo mingine iliyochezwa Novemba sita, Monaco imeendelea kupepesuka msimu huu licha ya kuwa na kocha mpya, ambapo katika mchezo wao dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji wameambulia kichapo cha mabao manne kwa nunge na kuwafanya waendelee kuburuza mkia kwenye kundi A wakiwa na alama moja kwenye michezo minne iliyocheza.

Nao Atletico Madrid wamewabugiza Borussia Dortmund mabao mawili kwa nunge ambapo timu hiyo inafikisha alama tisa sawa na Dortmund na hivyo ushindi huo wa Atletico unaiondoa rasmi Monaco kwenye ligi ya mabingwa msimu huu.

Kwingineko kwenye kundi B, FC Barcelona imejihakikishia kusonga mbele kwa hatua ya mtoano baada ya kulazimisha sare ya kufungana bao moja kwa moja na Inter Milan ya Italia.

Barcelona imefikisha alama 10 ambazo zinaweza kufikiwa na Inter Milan yenye alama saba na Tottenham Hotspur yenye alama nne ambapo miamba hiyo ya Hispania imebakiza michezo miwili dhidi ya PSV Eindhoven na mwingine ni dhidi ya Tottenham.

Katika kundi D, FC Porto imeinyuka Locomotiv Moscow mabao manne kwa moja huku Schalke 04 ikiibugiza Galatasaray mabao mawili kwa bila.

Leo Novemba saba, inapigwa michezo mingine nane ya makundi E mpaka H, ambapo kwenye kundi E Bayern wenye alama saba wanawaalika vibonde wa kundi lao AEK Athens na Benfica wanakipiga na Ajax.

Olympique Lyon ya Ufaransa inakipiga na TSG Hoffenheim ya Ujerumani huku Manchester City ikiialika Shakhtar Donetsk katika michezo ya kundi F huku CSKA Moscow watapepetana na AS Roma wakati Viktoria Plzen wakiwaalika mabingwa watetezi Real Madrid kwenye michezo ya kundi G.

Na Valencia wanapepetana na Young Boys huku kibibi kizee cha Turin, Juvetus wakiwa wenyeji wa mashetani wekundu kwenye michezo ya kundi H.