Nyota wa mchezo wa Tenisi kwa upande wa akina dada Naomi Osaka ameombwa radhi na kundi la vichekesho la A Masso la nchini Japan, baada ya kumkejeli nyota huyo anayeibukia kwa kasi kwenye Tenesi kuwa anapaswa kujichubua ili awe mweupe kidogo.
Kundi hilo lilitoa kauli hiyo likiwa hewani kwenye kipindi cha Televisheni siku ya Jumapili, saa chache baada ya Naomi Osaka kumshinda Anastasia Pavlyuchenkova wa Russia kwenye mashindano ya wazi ya Pan Pacific yanayofanyika mjini Osaka nchini Japan.
Kauli hiyo haikupokelewa vizuri na watu wengi nchini Japan na wapenda michezo ulimwenguni, ikionekana ni kauli ya kibaguzi kutokana na Naomi Osaka kuwa amezaliwa na mama Mjapan huku Baba yake akiwa ni mweusi ambaye ni raia wa Haiti.
Kutokana na kukosolewa vikali, kundi hilo la A Masso limesema kuwa linaomba radhi kwa maneno yaliyoumiza hisia za wengi na kuahidi kutorudia tena kufanya jambo kama hilo.
Hata hivyo, Naomi Osaka hajajitokeza hadharani kuelezea chochote kuhusu maneno hayo ya kejeli pamoja na msamaha alioombwa na kundi hilo linaloundwa na Wanawake Wawili.