Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limepata haki ya kutangaza mashindano ya kombe la FIFA la Dunia yatakayofanyika huko Qatar.
Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema kuwa, TBC itarusha mechi 28 katika Televisheni na katika mitandao yake ya kijamii na mechi nyingine 64 zitarushwa kupitia redio.
Amesema katika mashindano hayo ya Kombe la FIFA la Dunia yatakayoanza Novemba 20 hadi Desemba 18 mwaka huu, TBC itahakikisha inawapatia wasikilizaji wa redio na watazamaji wa Televisheni matangazo bora zaidi.
Dkt. Rioba amesema TBC imewahi kutangaza matangazo hayo katika Kombe la FIFA la Dunia mwaka 2010, 2014 na 2018, hivyo ina uwezo wa kutosha wa kuwapa wapenzi wa mpira burudani.