Kombe la dunia mwaka 2022 kuwa na timu 48

0
1796

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limesema kuwa ongezeko la timu kwenye michuano ya kombe la dunia inaweza kuanza kwenye michuano ya mwaka 2022 badala ya mwaka 2026 kama ilivyotarajiwa hapo awali.

Tayari maamuzi yameshapitishwa kuhusu kuongeza timu kutoka 32 hadi 48 na ilipangwa kuanza kwenye michuano ya mwaka 2026 itakayofanyika katika nchi za Marekani,Mexico na  Canada lakini sasa inavyoelekea ongezeko hilo litaanza kwenye michuano ijayo itakayofanyika nchini Qatar.

Rais wa FIFA, -Gianni Infantino amesema kuwa hilo linawezekana na sasa wako kwenye majadiliano na Qatar pamoja na washirika wao wengine ili kuona hilo linafanikiwa.

Infantino amesema kuwa FIFA itafanya kila linalowezekana ili kuona suala hilo linafanikiwa ili timu 48 zishiriki michuano hiyo ya kombe la Dunia ya mwaka 2022.

Pia Rais huyo wa FIFA amezungumzia mpango wake wa kuboresha michuano ya kombe la Dunia ya vilabu ambapo amesema kuwa anataka kuifanya michuano hiyo kuwa bora zaidi na inayopendwa na vilabu vyote duniani.