Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya soka (Taifa Stars) Adel Amrouche amesema, anategema kujenga historia mpya kwa Tanzania huku akiomba ushirikiano kutoka kwa Watanzania kwani wana mchango mkubwa katika maendeleo ya soka nchini.
Akizungumza mara baada ya hafla ya kutambulishwa jijini Dodoma, Amrouche amesema jukumu la pili ambalo atalibeba ni kuendeleza vipaji vya vijana.
“Lazima tulinde vipaji vyetu. Tuna wachezaji hapa Tanzania lakini ni muhimu wakapewa nafasi. Ninajua mara zote huwa ni kati ya wachezaji wa timu mbili kubwa, Simba na Yanga, lakini ni muhimu kuangalia wachezaji nchi nzima na kuwapa nafasi,” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Pindi Chana amesema Serikali imechukua jukumu kumlipa mshahara kocha Amrouche ili atekeleze majukumu yake kwa ufanisi na Watanzania wabaki wanamdai matokeo.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendeleza michezo yote na sio mpira wa miguu tu, ili kulitangaza Taifa, kutoa ajira na burudani kwa Watanzania.