Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameziagiza wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha kila shule ya Msingi na Sekondari inakuwa na mwalimu mmoja wa somo la michezo.
Dkt. Mpango ametoa agizo hilo alipokuwa akifungua Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Mashindano ya Umoja wa Michezo Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.
Amesema hatua hiyo itaimarisha michezo katika shule mbalimbali nchini na pia itawezesha kufundishwa kwa somo hilo bila kukosa.
“Hakikisheni wasimamizi wa elimu katika ngazi zote somo la michezo linazingatiwa.” Ameagiza Dkt. Mpango
Aidha, amehimiza shule mpya zinazojengwa kuanzia sasa kuwa na maeneo ya kutosha ambapo vitajengwa viwanja vya michezo.
“Maeneo hayo yaendane na upandaji wa miti kuzunguka viwanja hivyo ili wakati wa mchezo kuwepo na hewa safi”. amesema Dkt. Mpango
Makamu wa Rais amesema baadhi ya shule na taasisi binafsi zinafanya vizuri katika michezo akitolea mfano shule ya Fountain Gate ya jijini Dodoma iliyoshinda katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa.
“Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuboresha mashindano haya ya UMITASHUMTA na UMISSETA na kuunga mkono juhudi za michezo zinazofanywa nchini na niseme hapa hapa wasimamizi wa elimu ngazi zote motisha za wanafunzi katika michezo ziwepo.” Amesisitiza Dkt. Mpango