Kaseja kulamba Shilingi Milioni Kumi

0
759

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa ya timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars), Paul Makonda ameahidi kutoa Shilingi Milioni Kumi kwa Golikipa wa timu hiyo Juma Kaseja baada ya kufurahishwa na kiwango alichokionesha kwenye mchezo kati ya Stars na timu ya Taifa ya Burundi.

Kaseja ameingoza Stars kupata ushindi wa penati 3-0 dhidi ya Burundi huku akifuta penati moja na kuiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2022.

Katika dakika 90 za mchezo huo wa marudiano uliopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es salaam, timu hizo zilitoka sare ya kufungana goli 1-1.

Goli la Tanzania lilifungwa na mchezaji wa Kimataifa ambaye ni Nahodha wa Stars, – Mbwana Samatta katika dakika ya 29, huku lile la Burundi likifungwa katika dakika ya 45 ya mchezo huo na Abdul Fieston.

Baada ya kukamilika kwa dakika 90, zikaongezwa nyingine 30, lakini hata hivyo zilipomalizika dakika 120 magoli yalikua 1-1 na ndipo ikafuata mikwaju ya penati.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa mjini Bujumbura nchini Burundi, timu hizo zilitoka sare kwa kufungana goli 1-1.