Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Rais John Magufuli amesema kuwa, miongoni mwa changamoto kubwa zinazolikabili Taifa ni hujuma dhidi ya jitihada za Serikali, hujuma ambazo zimekua zikifanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema Tanzania.
Akizungumza mkoani Mwanza wakati wa ufunguzi wa majadiliano ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Magufuli amesema kuwa hujuma hizo zina lengo la kudhoofisha jitihada za Serikali za kulikomboa Taifa kiuchumi na kwamba watu ambao wamekua wakifanya hujuma hizo ni kwa maslahi yao binafsi.
Rais Magufuli amewaeleza Wajumbe hao kuwa, kuna baadhi ya watu kamwe hawataki kuona Serikali inadhibiti rasilimali zake ambazo katika siku za nyuma walikuwa wakizivuna na kuzisafirisha wanavyotaka bila kuhojiwa.
Zaidi ya hapo, watu hawa hawatakubali tutekeleze miradi mikubwa ya kimapinduzi itakayoharakisha maendeleo nchini ikiwemo bwawa la Nyerere, SGR au kufufua Shirika la ATCL, wasingependa tutoe elimu bure, wasingependa tupeleke umeme katika vijiji vyote na mengine mengi, wangependa tuendelee kuwategemea wao ilihali wao wanaishi kwa kutegemea rasilimali zetu”, amesema Rais Magufuli.
Wanatumia kila njia kufifisha jitihada zetu na kupenyeza ajenda zao, wakati mwingine wanatumia asasi za kiraia na Mashirika yasiyo ya Kiserikali na kujifanya wanatufundisha Demokrasia na haki za binadamu, wakati wao wenyewe wanavunja misingi hiyo kwa kujenga mifumo ya kinyonyaji, kuchochea machafuko na kuingilia uhuru wa Mataifa mengine, wakati mwingine, watajenga mazingira ya taharuki na kusema Ebola imeingia Tanzania ili mradi tu ionekane nchi haiko salama”, ameongeza Rais Magufuli.
Rais Magufuli ametumia majadiliano hayo ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kuwataka Watanzania wote watambue kuwa hujuma ndiyo changamoto kubwa katika mapito ya Taifa kuelekea ukombozi wa kiuchumi na kwamba wasiposimama imara, kujenga uzalendo na moyo wa kujitolea kwa Taifa, Serikali haitaweza kuikabili.