Klabu ya Inter Milan ya nchini Italia imemvua unahodha mshambuliaji wake Mauro Icardi, baada ya nyota huyo kugoma kusafiri na timu hiyo kwenye mchezo wa michuano ya Yuropa dhidi ya Rapid Vienna, akishikiza kupatiwa mkataba mpya na klabu hiyo.
Mkataba wa sasa wa mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Argentina kwenye dimba la Guissepe Meaza unamalizika mwaka 2021 na klabu hiyo ilikuwa kwenye mazungumzo ya mkataba mpya na mke wa Icardi,- Wanda Nara ambaye inasemekana ndiye wakala wake.
Tayari klabu hiyo imemtangaza mlinda mlango Samir Handanovic kuwa nahodha mpya wa kikosi hicho, na kocha wa Inter Milan, – Luciano Spalletti amesema kuwa maamuzi ya kumvua unahodha Icardi yalikuwa magumu na yenye kuumiza lakini hakukuwa na namna nyingine kwa ustawi wa klabu.
Icardi alijiunga na Inter mwaka 2013 akitokea Sampdoria na kukabidhiwa kitambaa cha unahodha mwaka 2015, na tayari ameifungia klabu hiyo mabao 122 katika michezo 208 aliyoitumikia klabu hiyo inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Seria A wakiwa alama 20 nyuma ya vinara Juventus.