Kocha mpya wa klabu ya AS Monaco, – Thierry Henry amesema kuwa kocha wa Manchester City, – Pep Guardiola atakuwa motisha kubwa kwake katika majukumu yake mapya ya ukocha nchini Ufaransa.
Henry ambaye alianza maisha yake ya soka la kiushindani kwenye klabu ya Monaco, amerejea kwenye klabu hiyo kama kocha baada ya klabu hiyo kumtimua kocha wake Leonardo Jardim kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo kwenye ligi.
Nyota huyo wa zamani wa Arsenal ambaye amewahi pia kuichezea FC Barcelona chini ya Guardiola amesena kuwa Pep ni muongozo mzuri kwake kutokana na mbinu alizonazo wakati mchezo ukiendelea na hata kabla ya mchezo.
Alipoulizwa kuhusu Mfaransa mwenzake Arsene Wenger ambaye chini yake alicheza kwa mafanikio makubwa, Henry amesema kuwa siku zote Wenger atabaki kuwa mtu muhimu kwake aliyemfanya kujua nini maana ya soka la ushindani na wanamahusiano mazuri na kuna baadhi ya vitu kutoka kwake atavitumia kwenye kazi yake ya ukocha.
Henry ambaye alikuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Ubelgiji, amesaini mkataba wa miaka mitatu na Monaco utakaofanya kuhudumu hadi mwezi June mwaka 2021 na mwaka 1997 aliisaidia Monaco kushinda taji la ligi ya Ufaransa na sasa anakibarua cha kuinasua timu hiyo kutoka mkiani na mchezo wake wa kwanza utakuwa dhidi ya Strasbourg Oktoba 20 mwaka huu kabla ya kumenyana na Club Brugge siku nne baadae kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya.