FIFA kujenga viwanja vya Soka Barani Afrika

0
920

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limetangaza mpango wake wa kutoa Dola Bilioni Moja za Kimarekani kwa ajili ya kujenga angalau kiwanja kimoja cha mpira kwa kila nchi ya Afrika, kiwanja ambacho kina viwango vya Shirikisho hilo.

Mpango huo umetangazwa na Rais wa FIFA, – Gianni Infantino katika mji wa Lubumbashi huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wakati wa maadhimisho ya miaka Themanini tangu kuanzishwa kwa Klabu ya TP Mazembe.

Infantino amesisitiza kuwa, FIFA inataka kuona Soka la Afrika linakua na kushamiri, hivyo itaendelea kushirikiana na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na Wadau mbalimbali ili kuinua kiwango cha Soka katika Bara hilo.

Rais huyo wa Shirikisho la Soka Duniani amesema kuwa, ili kufanikisha mpango wa kujenga angalau kiwanja kimoja cha Soka kwa kila nchi ya Afrika ambacho kina viwango vya FIFA, Shirikisho hilo litaomba kampuni mbalimbali pamoja na Wafanyabiashara wakubwa duniani kuchangia kiasi hicho cha fedha.