Zikiwa zimebaki saa chache kabla ya kuanza kwa fainali za 21 za kombe la FIFA la dunia hii leo Juni 13 wanachama 211 wa shirikisho la soka duniani -FIFA watapiga kura kuchagua nchi itakayoandaa fainali za kombe la FIFA la dunia za mwaka 2026 kwenye mkutano mkuu wa FIFA utakaofanyika jijini Moscow nchini Russia.
Baada ya kutokea utata na tuhuma za mlungula kwenye kupata wenyeji wa fainali za kombe la FIFA la dunia mwaka 2018 na 2022, FIFA imeahidi kuwepo na uwazi kwenye kupiga kura ili kupata nchi ya kuandaa fainali za mwaka 2026.
Nchi ya Morocco kutoka Kaskazini mwa bara la Afrika inapambana na nchi tatu za Marekani, Canada na Mexico ambazo zimeomba kuandaa michuano hiyo kwa ushirikiano.
Kampeni za Marekani na washirika wake, zinaongozwa na nyota David Beckham ambaye amesema nchi bora inastahili kupata nafasi hiyo ya kuandaa fainali za kombe la FIFA la dunia za mwaka 2026 huku Rais wa Marekani, Donald Trump akiongeza ushawishi wa nchi hizo za Kaskazini mwa Amerika kupata nafasi hiyo.
Morocco yenyewe imeahidi kuwa na miundombinu bora yenye kiwango cha juu na kuongeza kuwa fainali hizo zikifanyika nchini mwao zitakuwa fainali za bara la Ulaya na Afrika kwasababu nchi hiyo ipo karibu na bara la Ulaya.
Zoezi la upigaji kura litaendeshwa kwa kila nchi iliyoomba kuandaa fainali hizo kupewa dakika 15 za kuwasilisha mapendekezo yao kwa wanachama 211 na baadae zitapigwa kura huku wajumbe 22 wenye nguvu ndani ya FIFA wakizuiwa kupiga kura huku wakiwa hawana maamuzi yoyote ya kufanya juu ya uchaguzi huo.
Oscar Urassa
13 Juni 2018