Fainali za 21 za kombe la FIFA la Dunia kufanyika kama ilivyopangwa

0
244

Mtendaji Mkuu wa fainali za 21 za kombe la FIFA la Dunia, – Nasser Al-Khater amesema fainali hizo zilizopangwa kufanyika nchini Qatar mwaka 2022 zitafanyika kama zilivyopangwa baada ya nchi hiyo kufanikiwa katika chanjo dhidi ya virusi vya Corona.

Al-Khater ameliambia shirika la habari la AP la nchini Marekani kuwa, chanjo dhidi ya virusi vya Corona nchini Qatar imeonesha mafanikio makubwa na hivyo wana imani hadi kufikia mwaka 2022 watafanikiwa kuvidhibiti kabisa na maisha kurejea kama kawaida.

Mapema mwaka huu mlipuko wa virusi vya Corona ulisababisha mashindano kadhaa kufutwa yakiwemo yale ya mataifa ya Ulaya pamoja na michuano mikubwa ya Olimpiki iliyokuwa ifanyike Tokyo nchini Japan, na hivyo kuzua wasiwasi kuhusu kufanyika kwa fainali za kombe la FIFA la dunia ambazo kwa mara ya kwanza zitafanyika huko mashariki ya kati.

Tayari nchi ya Qatar imekamilisha ujenzi wa viwanja vitatu vya kisasa kati ya nane vitakavyotumika katika fainali hizo na kiwanja cha nne kijulikanacho kama Al Rayyan kipo mbioni kumalizika, na viwanja vinne vilivyosalia vitakamilika mwishoni mwaka 2021.

Tofauti na fainali zilizotangulia, fainali za kombe la FIFA la dunia za mwaka 2022 zitaunguruma mwishoni mwa mwaka ambapo kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Duniani – FIFA, fainali hizo zitaanza rasmi kuunguruma Novemba 21 na kufikia tamati Disemba 18 mwaka 2022.