Djokovic ashinda mashindano ya wazi ya Madrid

0
279

Nyota nambari Moja kwenye viwango vya ubora wa mchezo wa Tenisi duniani kwa upande wa wanaume Novak Djokovic ameshinda taji la mashindano ya wazi ya Madrid baada ya kumnyuka Stefano Tsitsipas wa Ugiriki kwa seti Mbili kwa bila kwenye mchezo wa fainali.

Djokovic ambaye alitinga fainali kwa kumtupa nje ya michuano hiyo mkongwe Rafael Nadal,  ametumia muda wa saa moja na dakika 32 kupata ushindi wa 6-3 na 6-4 dhidi ya kinda huyo mwenye miaka Ishirini  na kutwaa ubingwa huo kwa mara ya Tatu.

Akizungumzia ushindi huo Djokovic anasema kuwa ni wa muhimu sana kwake na utamuongezea kujiamini hasa baada ya kucheza kwa kiwango cha chini tangu yalipomalizika mashindano ya wazi ya Australia na anaamini atakuwa bora zaidi na kurejea katika kiwango chake cha siku zote.

Kwa upande wa wanawake, taji hilo la mashindano ya wazi ya Madrid limenyakuliwa na Kick Bertes wa Uholanzi aliyemnyuka Simona Halep wa Romani kwa seti mbili kwa bila za ushindi wa 6-4 na 6-4 katika mchezo wa fainali na kumfanya Halep kupoteza nafasi ya kupanda hadi katika nafasi ya kwanza kwenye viwango vya ubora.